LICHA ya kuwepo kwa wafanyabiashara wachache wa sukari wasio waaminifu mkoani Mwanza kupandisha bei ya bidhaa hiyo kwa asilimia 22 kutoka Shilingi 2,300 hadi 2,800 kwa kilo moja, uzalishaji wa sukari umepanda hadi kufikia tani 326,000 kwa mwaka 2016/2017. Kupanda kwa kiwango hicho cha uzalishaji sukari nchini kumebainishwa na Mwenyekiti wa mfuko wa maendeleo wa sekta ya sukari Tanzania (SIDTF), Deo Lyatto, wakati wa kikao cha wataalamu wa sukari cha kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Kwa upande wa wazalishaji wa sukari na wakulima wa miwa nchini na nje wameishauri serikali kutoa ushirikiano wa kutosha katika sekta hiyo ili kujenga uchumi na kuwezesha adhima ya serikali kuwa na nchi ya viwanda. Naye Mkurungenzi wa bodi ya sukari nchini, Henry Semwanza, alisema huu ni muda muafaka kwa wazalishaji wa sukari kuongeza jitihada katika kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuuza kwa bei ya chini ambayo wanachi wa hali ya chini waweze kumudu bei hiyo.