MSANII Nikki Aiweka Sawa Kauli yake ya Uchunguzi wa Ajali iliyoua 32

Msanii wa muziki wa hip hop, Nikki wa Pili amefafanua kauli yake ya uchunguzi ufanyike katika ajali iliyoua 32 Arusha baada ya kudai kuna baadhi ya watu wameshindwa kuielewa kauli yake hiyo.


Rapa huyo amedai kuwa ni jambo la utu kama tatizo litajulikana na kufanyiwa marekebisho kwa vitendo na siyo kuhukumu watu au kumtafuta mchawi nani kipindi hiki, huku akitaka asinukuliwe vibaya.

“Nasikitika watu wameninukuu vibaya sana niliposema uchunguzi ufanyike wengine wameniponda lakini sijachukia kwani hawajanielewa,” Nikki alikiambia kipindi cha Planet Bongo cha EA Radio. “Uchunguzi ukifanyika sina maana ya kumhukumu mtu mmoja hapana bali tuweze kujifunza. Watu wengi waliokusanyika uwanjani kuaga walimu na wanafunzi wameonyesha utu lakini pasipo tukio hili kuchunguzwa utu wao utakua hauna thaani kwani matatizo haya yatajirudia mara kwa mara,”

Aliongeza, “Inawezekana kuwa mikanda ilikosekana kwenye ‘bus’ walilokuwa wamepanda wanafunzi na walimu wa Lucky Vicent Academy au mwendo haukuwa mzuri lakini tatizo linaweza kuwa hali ya hewa hivi ni vitu ambavyo vikifanyiwa uchunguzi vinaweza kutukumbusha tabia zetu na tutajifunza wakati mwingine,”

Katika hatua nyingine Nikki amewaona watu wanaoweka mitandaoni picha za ajali na kusema kuwa ni vitendo vya udhalilishaji na kuongeza kwamba zipo njia nyingi za kutoa taarifa kwenye mitandao lakini siyo kwa ku- ‘share’ picha za ajali ambazo watu wanakuwa wameumia vibaya.

Comments