Hizi Hapa Sababu za Wanaume Wengi Kutokuoa Siku Hizi..!!!
Kumekuwa na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii kwamba imekuaje
vijana wa kiume wamekuwa ni waongo sana hasa linapokuja swala la kuoa?
Kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo idadi ya wanaume
wanaoogopa kuoa inazidi kuongezeka. Utakuta wapenzi wanaambiana kwamba
wanapendana na kuahidiana kuwa wataoana, lakini kitakachotokea baada ya
hapo ni mwanaume kuanza kupiga chenga kwa visingizio lukuki.
Kwa nini hali hiyo hutokea?
Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja juu ya tatizo hilo, lakini
yapo mambo ambayo yanaweza kutupa angalau tafakuri. Nitajaribu
kudadavua baadhi ya sababu zinazowafanya wanaume siku hizi kukwepa
kuingia katika taasisi ya ndoa:
1 Ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano:
Hapa nawazungumzia wale watoto wa kiume waliolelewa malezi ya upande
mmoja yaani walilelewa na mama peke yao. Sina maana ya kudharau au
kutweza malezi ya mama, la hasha, lakini ni vyema mkafahamu kwamba kuwa
na baba asiye na malezi mazuri si sawa na kutokuwa na baba. Na ndio
maana nikasema ukosefu wa mtu wa kumchukulia kama mfano. Achilia mbali
aina ya malezi atakayoyapata kwa familia yawe mazuri au mabaya lakini
lazima kutakuwa na tabia za kiume zitakazoakisi malezi ya mtoto wa kiume
katika familia husika. Watoto waliolelewa na mama peke yao kuna kitu
huwa wanakosa, kwani wanakuwa hawana mtu wa kumchukulia kama mfano kwa
upande wa jinsia ya kiume na hapo ndipo hujikuta wakijifunza wenyewe
namna ya kuongea na kutenda kama wanaume kwa sababu katika makuzi yao
hawakupata fursa ya kuwa karibu na baba zao. Kwa kuwa siku hizi kuna
kundi kubwa la kina mama ambao wamejikuta wakiachiwa mzigo wa malezi ya
watoto, baada ya aidha kuachwa na waume zao au kuzalishwa na kutelekezwa
(Single mothers), na hapo ndipo tunaposhuhudia mtoto wa kiume anapokua
kwa umri na kimo huku akiwa hana mtu wa kumuangalia kama mfano wa mume
anavyotakiwa kuwa katika familia zaidi ya kujifunza mambo hayo kupitia
katika TV, senema au miziki. Wanaume waliopitia malezi ya aina hii
huchelewa sana kuoa kwani huyaangalia maisha ya ndoa kwa namna ya
kujaribu na ndipo hapo wengi huishia kuishi kinyumba na wanawake kwa
ajili ya kutaka kujifunza namna ya maisha ya ndoa yanavyotakiwa kuwa na
ndio sababu huchukua muda mrefu kufanya maamuzi. Na mara nyingi huishia
kubadilisha wanawake kutokana na kutokuwa na uhakika wa kile
wanachokitafuta.
2 Mgogoro wa kiuchumi:
Kuna kundi kubwa la vijana siku hizi hawana ajira au hawana uhakika na
kipato. Ukweli ni kwamba hakuna mwanaume atakayependa kujiingiza kwenye
ndoa wakati hana kazi au hana uhakika na kipato chake. Na hiyo ni
kutokana na wanawake wengi siku hizi kuonekana kujali zaidi wanaume
wenye uhakika na kipato. Hii misemo ya wanawake ya kebehi dhidi ya
wanaume wasio na ajira au kipato, kama vile “mwanaume suruale” ina
mchango mkubwa sana katika kuwafanya wanaume kukwepa kuoa iwapo hawana
ajira au hawana uhakika na kipato chao.
3 Wanawake wengi kuwa na kiwango cha elimu ya juu:
Siku hizi wanawake wengi wameibuka katika kutafuta elimu ya juu kwa
juhudi kubwa. Idadi ya wanawake wanaojiunga na vyuo vikuu ni wengi
tofauti na ilivyokuwa zamani. Na hiyo ni kutokana na wazazi wengi
kubadili mtazamo wao juu ya mtoto wa kike. Zamani mtoto wa kike
alichukuliwa kama kitega uchumi. Kwa maeneo ya vijijini na katika
familia masikini, watoto wa kike walikuwa wanatazamwa kama, ‘biashara ya
kesho’ ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ilikuwa
ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu. Lakini tofauti na
zamani siku hizi hata kule vijijini kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa
kumsomesha mtoto wa kike hadi elimu ya juu. Kutokana na mwamko huo
wanawake wengi wamejikuta wakiona elimu kama kimbilio pekee la kuepukana
na mfumo dume. Mwanamke gani atakubali kunyanyaswa na mwanaume akiwa na
elimu yake na labda pia akiwa na kazi yake yenye mshahara na marupurupu
ya kutosha, naamini watakuwa ni wachache sana ambao hawajiamini au
waliathiriwa na malezi. Kwa upande wa wanaume nao, wamejikuta
wakiwaogopa wanawake hawa wenye elimu ya juu kwa hofu ya kuzidiwa kipato
na labda kukosa sauti kama mwanaume na hiyo inatokana na ego tu.
4 Wanaume huwaona wanawake kama tishio wanapokuwa na mafanikio makubwa kifedha:
Inaweza kutokea mwanaume anaweza kuwa na uhusiano na mwanamke ambaye
labda tu nisema ni mbangaizaji. Wakati huo anaweza kuahidi kufunga ndoa
na mwanamke huyo, lakini iwapo itatokea mwanamke huyo akapata mafanikio
kibiashara na kuinuka kifedha. Kama mwanamke asipokuwa makini anaweza
kusababisha mwanaume huyo akaingia mitini. Sababu kubwa hapo inaweza
kuwa ni hofu ya kuogopa kuongozwa na mwanamke. Kumbuka kwamba mfumo dume
bado umetawala vichwani mwa wanaume wengi kutokana na malezi. Mwanaume
asiyejiamini ni vigumu sana kwake kuoa mwanamke aliyemzidi kipato. Kwa
sababu akifanyiwa jambo dogo tu, inakuwa kama ametoneshwa. Atahisi
kutaka kutawaliwa na mwanamke huyo. Jambo ambalo wanawake wanatakiwa
kulifahamu ni kwamba kila mwanaume anataka kutambuliwa na kuheshimiwa
kama shujaa kabla ya kumfuata msichana. Iwapo utakuwa umesimama iwe ni
kifedha au kielimu pale unapotafuta kupata mwenza, inabidi ujishushe
sana la sivyo utadoda.
5 Wanaume wengi siku hizi wana hofu ya majukumu, hasa ya kulea watoto:
Kutokana na malezi yao au kile wanachokijua kuhusu watoto, baadhi ya
vijana huamini kwamba, kulea watoto ni jambo gumu sana. Lakini wengine
wanaamini kwamba, hata mke anapaswa kulelewa kama ilivyo kwa mtoto.
Hivyo wanaamua kutafuta kwanza uwezo ambao haupatikani kiurahisi. Kuna
wengine, ambao wamefundishwa au kuelekezwa na mila na desturi zao
kwamba, kabla hawajaoa, ni lazima wawe na nyumba kwanza, tena kwao. Kwa
hiyo, hawa hadi waje wapate uwezo wa fedha wanakuwa wameshachelewa.
6 Kuna baadhi ya wanaume, maisha bila ya ndoa wanayaona kuwa ndiyo bora kuliko yale ya ndoa:
Kuna baadhi ya wanawake hujirahisisha sana kwa wanaume. Siku hizi ni
jambo la kawaida sana kukuta mwanaume anaishi na mwanamke bila ndoa,
wenyewe wanaita Trial Marriage. Na hapo ndipo unapokuta wanaume hawaoni
tena umuhimu wa kuoa. Sasa kama mwanamke anaweza tu kuishi na mwanaume
bila ya ndoa na mwanaume huyo akapata huduma zote kutoka kwa mwanamke
huyo, unadhani ni kitu gani kitamvuta kufunga ndoa. Jambo lingine ni ile
dhana kwamba maana ya ndoa ni tendo la ndoa. Siku hizi wanaume wengi
wamejikuta wakiwa hawahitaji tena kuoa kwa sababu tendo hilo
linapatikana kiurahisi tofauti na zamani. Siku hizi inawezekana kabisa
kumtongoza binti leo na kupata tendo siku hiyo hiyo….. Na hapa
siwazungumzii makahaba. Nawazungumzia mabinti zetu ambao wengine
ukiwaona ni watu wa kuheshimiwa ukiwaangalia kwa nje lakini kwa ndani
hawana lolote, vijana wa siku hizi wenyewe huwaita maharage ya Mbeya.
Kuna sababu nyingi zinazotajwa kusababisha wanaume siku hizi kujivuta
sana katika kufanya maamuzi ya kutafuta mwenza. Lakini hizo chache
nilizozitaja zina mchango mkubwa.
Comments
Post a Comment